Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kampeni za kususia bidhaa za kampuni za kimataifa zinazounga mkono Uzayuni zimejitokeza kama nyenzo ya mapambano na ya kipekee katika shughuli za asasi za kiraia kwa ajili ya kuunga mkono haki ya Wapalestina, Katika muktadha huo, wanaharakati nchini Tunisia wamejiunga na “kampeni ya kimataifa” inayolenga kampuni na taasisi zinazotuhumiwa kuunga mkono au kushirikiana na utawala wa Kizayuni, katika mfumo wa mshikamano mpana na wananchi wa Palestina.
Kususia ikiwa kama Chombo cha Kimkakati cha Shinikizo
Katika muktadha huo, “Sadiq Ammar”, mwenyekiti wa “Muungano wa Tunisia wa Kuunga Mkono Haki ya Palestina”, katika mahojiano na tovuti ya habari ya “Al-Ahed”, alizungumzia asili ya kususia pamoja na vipengele vyake vya kihistoria na vya mapambano, na akasisitiza kwamba; harakati hii bado inaendelea duniani kote.
Alifafanua kwamba; silaha hii si ubunifu wa kisasa, bali ni urithi wa mapambano uliokuwa ukitumika tangu enzi za ukoloni, alirejelea mafanikio ya Gandi katika kuwalazimisha wakoloni Waingereza kukubali hali halisi kupitia kususia kampuni za nguo, jambo lililosababisha hasara kubwa kwao na kuzilazimisha kampuni zao nyingi kurejea Uingereza.
Ammar alisisitiza kwamba; leo kususia ni mojawapo ya nyenzo nyingi za muqawama — zikiwemo siasa, fikra na utamaduni — ambazo zote hukusanyika katika lengo moja la pamoja, nalo ni “kupigania uhuru”.
Alibainisha kwamba “Muungano wa Tunisia wa Kuunga Mkono Haki ya Palestina” tangu kuanza kwa vita vya Oktoba, umeshiriki katika kuandaa mikusanyiko na harakati nyingi za uwanjani kwa ajili ya kupaza sauti dhidi ya kampuni zinazounga mkono utawala wa Kizayuni. Pia umewataka wananchi wa Tunisia na mataifa mengine ya Kiarabu kuikubali njia hii kama aina ya kutetea haki ya Palestina, licha ya kufahamu ugumu uliopo katika kuifuata.
Silaha ya Mataifa
Nchini Tunisia, kususia kumevuka mipaka ya kuwa tabia ya kawaida ya matumizi na kuwa sehemu halisi ya mwamko wa umma wa wananchi wa Tunisia pamoja na msimamo wa kimaadili na kisiasa unaotokana na kuunga mkono suala la Palestina. Katika miaka ya hivi karibuni, kususia kumegeuka kuwa chombo cha amani cha shinikizo kinachoonyesha upinzani wa Watunisia dhidi ya aina yoyote ya kuhalalisha mahusiano na utawala wa Israeli au kuunga mkono ukaliaji wa mabavu wa Israeli.
Wanaharakati nchini Tunisia wanaamini kwamba; kususia hakulengi bidhaa pekee, bali lengo lake ni kumuwekea adui mzingiro wa kimwili na wa kimaadili pamoja na kumuelimisha mtumiaji kwamba; kila “dinari” inayotumiwa inaweza kuwa na mchango katika kufadhili sera ambazo dhamiri ya pamoja ya wananchi inazikataa.
Kampuni Zinazolengwa Nchini Tunisia
Kampeni za kususia nchini Tunisia kwa kawaida zimejikita katika kampuni zenye mikataba ya “franchise” (leseni ya biashara) na chapa za kimataifa zinazotuhumiwa kuunga mkono ukaliaji wa mabavu au ambazo zimeekeza moja kwa moja kwao. Miongoni mwa majina maarufu zaidi yaliyolengwa katika vipindi vya karibuni vya wito wa kususia ni “Carrefour”, ambayo inahesabiwa kuwa mojawapo ya minyororo ya maduka yaliyolengwa zaidi. Kampeni hizi zinaituhumu kampuni hiyo kuwa na uhusiano na makundi yanayounga mkono ukaliaji wa mabavu; ingawa matawi yake ya ndani hujaribu kujitenga na misimamo ya kampuni mama kwa kusisitiza kwamba wafanyakazi na uongozi wao ni Watunisia.
Kampuni zinazolengwa mara nyingi hujaribu kupunguza hasira za umma na kuhifadhi sehemu yao katika soko kwa kutoa taarifa za ufafanuzi au kuendesha kampeni za kutoa misaada ya kibinadamu kwa Ghaza, jambo ambalo lenyewe linaonesha athari halisi ya kampeni za kususia katika faida zao.
Ripoti za kiuchumi zinazofuatilia soko la Tunisia zinaonyesha kwamba; kampeni za kususia zimekuwa na athari ya wazi na zimesababisha kupungua kwa mauzo; kiasi kwamba baadhi ya chapa za kimataifa zimeshuhudia kushuka kwa kiwango kikubwa katika takwimu zao za biashara, hali ambayo katika vipindi fulani imefikia asilimia za kutia maanani na kuzilazimisha kuchukua hatua za kujilinda.
Vilevile, mwelekeo wa kutumia bidhaa mbadala za ndani na bidhaa za viwanda vya Tunisia umeongezeka, jambo ambalo wataalamu wa mwongozo wa matumizi wamelitaja kuwa ni hatua chanya katika kuimarisha uchumi wa taifa.
Kwa sasa, kususia kumegeuka kuwa suala la “maoni ya umma”, ambapo wanaharakati wanakusanya na kuthibitisha nyaraka kuhusu uhusiano wa kampuni mbalimbali na wavamizi, na wanatoa wito wa kuanzishwa utekelezaji wa sheria zinazoharamisha kuhalalisha mahusiano na utawala wa Kizayuni.
Maoni yako